#ZIFAHAMU: Sababu 4 za kwa nini haupungui uzito

Yapo mengi yanayozungumzwa kuhusiana na jinsi ya kupunguza uzito wa mwili, mengine ni ya kidaktari, kiimani, kitamaduni na mengineyo.

Wapo baadhi ya watu ambao hulalamika kuwa japokuwa wanafanya mazoezi na kula mlo kamili bado uzito wa miili yao unashindwa kupungua.

Hatahivyo wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kama mazoezi, mlo kamili na jitihada nyingine unazofanya kupungua hazizai matunda, basi hizi ndizo sababu zake

1. Haujabadilisha mlo wako

Mazoezi yanaendana na kula mlo bora ili kwamba uzito uwe kwenye hali inayotakiwa. Acha kula vyakula vya mafuta kama chipsi, burger na vinginevyo. Ukifanya mazoezi unakata mafuta ya mwili hivyo kama unaendelea kula mafuta kwa kiwango cha juu basi unafanya kazi bure.

Pia inaelezwa kuwa ni hatari mtu anayetaka kupungua akaruka milo yake, mfano kuamua kula wakati wa usiku tu, kinachofanyika ni kwamba ukifika wakati wa kula baada ya siku nzima kukaa njaa, unakula chakula kingi, kwani mwili unafidia chakula ulichotakiwa kula asubuhi na mchana.

Wataalamu wanashauri kutoruka milo, bali kula kwa kiasi na kula milo yenye virutubisho vinavyohitajika mwilini.

2. Haupati muda wa kutosha kulala

Kama unaamua kutumia muda wako wa kulala ukifanya mazoezi unakosea. Kutokulala kutakusabishia uchovu zaidi ambao utakufanya ushindwe ku-focus kwenye majukumu yako.

Wataalamu wanashauri kulala kabla ya kwenda kufanya mazoezi. Hii itasaidia misuli yako na mwili kupona na kurekebika tayari kwa shughuli nyingine.

3. Unafanya mazoezi zaidi ya inavyotakiwa

Inaelezwa kuwa kufanya jambo zaidi ya inavyotakiwa huwa na madhara, na hii kanuni pia inatumika katika mazoezi.

Mtu akizidisha mazoezi anadhoofisha misuli na hii inasababisha fatiki ya mwili. Mwili unapokuwa umechoka, unapunguza kazi yake ya kuchoma mafuta.

4. Haubadilishi aina ya mazoezi

Wataalamu wanaeleza kuwa mwili una tabia ya kuzoea kitu ambacho unakipitia jambo linalosababisha kutokuwa na ufanisi kwa eneo husika.

Kufanya mazoezi ya aina moja kunaweza kusababisha matokeo kuwa yasiyoridhisha, hivyo unashauriwa kubadilisha aina ya mazoezi unayofanya. Na pia sio lazima kufanya mazoezi kila siku.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*